Mbunge wa eneo bunge la Borabu Ben Momanyi amejitokeza kuitaka serikali ya kitaifa kujenga kituo cha kuwakumbuka wanajeshi waliouliwa kule Somalia, mahali ambapo majina ya wanajeshi hao yatakapoandikwa kama njia mojawapo ya kuwakumbuka. 

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akihutubia wakazi wa Omonono siku ya Alhamisi, Momanyi alisuta vikali hatua ya wizara ya ulinzi na mkuu wa majeshi nchini kuendelea kusitiri idadi kamili ya wanajeshi waliouwawa kule Somalia mapema Ijumaa wiki iliyopita, huku akihoji kuwa iwapo kituo hicho kitajengwa hiyo itakuwa njia mojawapo ya kuwapa heshima wanajeshi hao.

"Ni jambo la aibu kwamba wizara ya ulinzi inaendelea kusitiri idadi ya wanajeshi waliofariki kule Somalia na inafaa watangaze idadi hiyo ili waondoe hofu inayoendelea kuwakumba wakenya na itakuwa vizuri iwapo serikali itajenga kituo cha kuwakumbuka wanajeshi waliouliwa huko Somalia," alisema Momanyi. 

Momanyi aidha alisuta vikali mapendekezo ya baadhi ya wanasiasa nchini wanaotaka wanajeshi kuondolewa kule Somalia ili kulinda mipaka ya taifa akisema kuwa idadi ya wanajeshi wanao hudumu kule Somalia inafaa kuongezwa ili kukabili kundi haramu la wanamgambo wa Alshabaab. 

"Kundi hili haramu la Alshabaab limekuwa hatari kwa usalama wa taifa hili na pendekezo la kuwaondoa wanajeshi wetu kule Somalia halitakuwa hatua nzuri na ndio maana wanajeshi wetu waendelea kuwakabili wanamgambo hao kule Somalia hadi pale tutakapo waangamiza," alisisitiza Momanyi.