Share news tips with us here at Hivisasa

Wafanyibiashara katika eneo la Olympic mtaani Kibera wanakadiria hasara baada ya moto kuzuka Jumapili usiku katika mojawapo ya maduka yaliyoko eneo hilo.

Inadaiwa kuwa moto huo ulisababishwa na mlipuko wa mitungi ya gesi katika mojawapo ya duka la kuuza gesi lililoko maeneo hayo. Takriban maduka kumi yalichomeka huku wafanyibiashara hao wakipoteza kiasi kikubwa cha bidhaa kwani hawakupata fursa ya kuokoa bidhaa zao.

‘‘Tulisikia sauti ya mlipuko saa sita usiku kutoka nje tulipata moto umezuka,’’ alisema mmoja wa walioshuhudia kisa hicho.

Aidha kuwasili kwa wazima moto katika eneo la mkasa kulisaidia pakubwa kwani waliweza kukabiliana na moto huo uliokuwa ukisambaa kwa haraka na kusababisha maafa zaidi.

‘‘Wazima moto walifika kwa haraka wakazima moto huo lakini sisi kama wafanyibiashara tumekadiria hasara kubwa na tumepoteza bidhaa za bei ghali,’’ alisema mmoja wa wafanyibiashara aliyeathirika na mkasa huo.

Kisa cha moto katika eneo la Olympic kimetokea siku chache tu baada ya mkasa mwingine wa moto kutokea katika soko la Toi.