Share news tips with us here at Hivisasa

Vuguvugu la Mombasa Republican Council (MRC) limewahimiza wakaazi wa Pwani kujitokeza kwa wingi na kujisajili kama wapiga kura, wakati huu ambapo Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC inaendelea na zoezi la kuwasajili wapiga kura kote nchini.

Akizungumza katika eneo la Kaloleni kaunti ya Kilifi siku ya Jumanne, naibu msemaji wa kundi hilo, Richard Lewa, alisema kuwa njia ya pekee itakayowawezesha Wapwani kuwachagua viongozi watakaohakikisha kuwa wanapata haki zao za kidemokrasia ni kuchukua kura na kushiriki uchaguzi ujao.

“Wapwani tumesahaulika sana. Wakati umefika tuchukue kura ili katika uchaguzi ujao tuweze kufika kwenye debe na kuwachagua viongozi waadilifu,” alisema Lewa.

Awali kulizuka madai kuwa wanachama wa MRC walikuwa wamepanga kuvuruga shughuli hiyo katika eneo la Pwani hususan katika sehemu ambazo ni ngome zake, lakini Lewa ameyataja madai hayo kama yasiyo na msingi na kuwahimiza wakaazi kujitokeza kujiandikisha.

Awamu ya kwanza ya zoezi la kuwasajili wapiga kura ilianza tarehe 15 mwezi wa Februari na unatarajiwa kutamatika tarehe 15 mwezi huu.