Share news tips with us here at Hivisasa

Afisa anayesimamia usajili wa watu kwenye kaunti ndogo ya Rongai Bi Emilly Nyaga, amedokeza kwamba ofisi yake inakabiliwa na tatizo wakati wa utoaji wa vitambulisho kwa Wakenya kutoka kaunti zingine.

Alieleza kuhangaishwa na shule za msingi katika kaunti ndogo za Rongai, kwa kutoa vyeti ghushi kwa watu wanaotafuta vitambulisho vya kitaifa.

Akizungumza na mwandishi huyu Alhamisi, Bi Nyaga alisema kila wanapofanya ukaguzi wa watu wanaotaka vitambulisho, jamii za kutoka mpakani mwa Kenya haswa jamii ya Waturkana huwa na wakati mgumu kwa sababu ya ukosefu wa stakabadhi za kuonyesha kwamba wao ni Wakenya.

“Katika kazi yetu ni lazima tuhakikishe wewe ni Mkenya kwa kutoa cheti cha ubatizo, cheti cha kuonyesha ulisomea wapi, ama kile cha kuzaliwa,” alisema Bi Nyaga.

Hata hivyo alisema kwamba shule nyingi za eneo hilo zinatoa stakabadhi ghushi kwa watu wasio nazo, hali inayohatarisha sio tu utendakazi wa ofisi yake, mbali pia usalama wa taifa.

“Ofisi yetu imekabiliwa na shida kubwa kuhusu stakabadhi bandia kutoka kwa shule hizo, haswa ile ya msingi ya Kampi ya Moto na pia ya Magare. Tumekamata hata mhubiri mmoja bandia anayetoa cheti ghushi cha ubatizo, na tukikataa kuwasajili wanasema tunaitisha hongo,” alisisitiza.

“Sasa tunashirikiana na maafisa wa polisi kuchunguza, na kutumia pia vyombo vya habari ili kukamata wahusika,” aliongeza.

Kati ya waliokiri kufaidi na utoaji huo haramu wa vyeti na kudanganya miaka ni Alice Akiru ambaye cheti alichotoa shuleni humo kinaonyesha alijiunga na shule hiyo mwakani wa 1986, na kuondoka mwakani wa 1987.

Mwandishi huyu aliwasiliana na mwalimu mkuu wa shule ya Magare Stephen Chesire ambaye alisusia kuzungumzia jambo hilo.

Penina Chelimo mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Kampi ya Moto alikanusha habari hizo akisema zinapotosha.