Idara ya Trafiki katika Kaunti ya Nakuru imetoa onyo kwa wanaoendesha magari yao wakiwa walevi.
Idara hiyo imetangaza vita dhidi ya madereva walevi huku ikikariri kwamba itatumia kifaa aina ya ‘Alcoblow’ kinachopima kiwango cha pombe ambacho dereva amebugia, kwenye barabara zote za Nakuru.
Kupitia kwa afisa mkuu wa trafiki wa eneo la Nakuru Mary Omari, idara hiyo pia ilisema kuwa hatua hiyo inalenga kurejesha usalama barabarani haswaa msimu huu wa krismasi.
Akizungumza kwenye mahojiano na mwandishi huyu afisini mwake katika makao makuu ya Idara ya Trafiki mjini Nakuru siku ya Ijumaa Omari alisema operesheni hiyo itaanzishwa kutokana na ripoti kwamba baadhi ya madereva wanaendesha magari wakiwa walevi.
Omari alisisitiza kwamba oparesheni hiyo itaendelezwa usiku na mchana kwa kuwa wamegundua kuwa baadhi ya watu wanabugia vileo na kisha kuendesha magari hayo wakiwa walevi hata nyakati za mchana.
‘Wakati huu wa msimu wa krismasi na shamrashamra za Disemba, tutakuwa barabarani tukipima viwango vya pombe ambavyo madereva wamebugia. Tutatumia kifaa cha ‘Alcoblow’ na yeyote atakayepatikana akiwa amebugia kiwango cha pombe kilichopindukia, atachukuliwa hatua za kisheria,” alisema Omari.
Wakati huo huo, Omari alisema kwamba watajibidiisha kuhakikisha kuwa idadi ya ajali za barabarani imepungua haswaa wakati wa msimu wa sherehe za krismamsi ambapo ajali nyingi hushuhudiwa.