Mwanaume mmoja wa umri wa makamo anayekabiliwa na shtaka la mauaji alifikishwa mbele ya mahakama ya Nakuru siku ya Jumanne .
Inadaiwa kwamba mnamo Disemba 25, 2015, Gerald Wasike alimuua Jane Wahito mjini Elburgon baada ya wawili hao wanaorifiwa kuwa wapenzi kwa wakati huo kuzozana.
Mshtakiwa anadaiwa kumgonga Jane Wahito kwa rungu kichwani hadi akafa baada ya kumshuku kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamme mwingine.
Hata hivyo, Gerald Wasike aliyefikishwa mbele ya jaji Mary Odero wa mahakama kuu ya Nakuru alikiri shtaka hilo akijitetea kuwa alikuwa mlevi na ni baada ya kuchukua simu ya marehemu na kupitia jumbe zake ambapo aligundua jumbe zilizoashiria alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamme mwingine , hatua iliyompelekea kujawa na hasira na kutekeleza kitendo hicho.
Pamoja na hayo, aliomba mahakama kumsamehe na kumwachilia huru akisema haikuwa mapenzi yake kumuuwa mwanamke huyo .
Jaji Mary Odero anayesikiza kesi hiyo hata hivyo aliagiza Wasike arejeshwe rumande hadi kesi dhidi yake itakaposikizwa tena mwezi Aprili tarehe 4.