Mshukiwa mwingine wa mauaji ya wanabiashara wa ngono amekamatwa na kufikisha wawili idadi ya waliokamatwa.
Kibet Kiprop mwenye umri wa miaka 28 alikamatwa wakati akitibiwa katika hospitali ya Nakuru level five baada ya kupatilizwa kichapo na umati wa watu wakati akijaribu kuiba pikipiki.
Kulingana na habari za kijasusi, Kibet ni mshukiwa dhidi ya mauaji ya Grace Wangari ambaye mwili wake ulipatikana kwenye chumba cha malazi cha Tumaini mwezi jana tarehe nane.
Kiprop alidaiwa kutoroka wakati huo na kwenda Isinya na alirudi Nakuru wiki jana.
Hayo yanajiri wakati ambapo maafisa wa urekebishaji tabia wametakiwa kuandaa taarifa katika kesi ambapo mshukiwa wa kwanza wa mauaji hayo ya makahaba Aston Wachira anataka kuachiliwa kwa bondi.
Amri hiyo ilitolewa na jaji wa mahakama ya juu Maureen Odero Jumatatu, wakati ombi la kuachiliwa kwa bondi lilifikishwa mbele yake.
Wiki moja iliyopita afisa wa upelelezi alikuwa amepewa makataa ya siku saba kutoa hisia zake kuhusu ombi la mshukiwa kupitia wakili wake Michael Wabomba, lililotolewa wakati kesi hiyo ilisikilizwa Februari nane.
Kesi hiyo itafikishwa mahakamani tena mnamo tarehe 7, mwezi Machi.