Mahakama kuu ya Mombasa imemuachilia huru mshukiwa wa ubakaji aliyefkuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani.
Mshukiwa, James Nyamai, alikabiliwa na madai ya kujaribu kumbaka mtoto wa miaka nane katika eneo la Changamwe mnamo Marchi 2, 2013.
Akitoa uamuzi wa kuachiliwa kwake siku ya Jumanne, jaji katika mahakama ya Mombasa, Martin Muya, alisema kuwa ushahidi uliotolewa dhidi ya madai hayo hauambatani, na kuonyesha kuwa mshukiwa huyo hakuwa na njama ya kutekeleza ubakaji.
Aidha, aliongeza kuwa kifungo alichopewa mshukiwa huyo na mahakama ya chini jijini Mombasa, si cha haki, ikizingatiwa ushahidi uliotolewa si wa ukweli.
Hatua hii inajiri baada ya James Nyamai kukata rufaa ya kupinga kifungo cha miaka 15 alichopewa katika mahakama ya chini.