Maafisa wa kupambana na ugaidi katika kaunti ya Mombasa wanamchunguza mshukiwa mmoja wa ugaidi anayeaminika kumiliki zaidi ya bunduki sita na kuwapa vijana kutekeleza uhalifu mjini Mombasa.
Kulingana na Kamishna wa kaunti ya Mombasa Nelson Marwa, mshukiwa huyo anayefahamika kwa jina Salim Islam amekuwa akishirikiana na vijana na kuwahangaisha wakazi wa mjini Mombasa kwa kutumia bunduki anazomiliki, na kukiuka agizo la serikali la kutotumia bunduki kinyume cha sheria.
Akiongea na wanahabari baada ya kukagua shughuli za utoaji huduma kwa wananchi katika kituo cha Huduma Mombasa siku ya Jumanne, Marwa amesema kwamba mshukiwa huyo atazidi kuzuiliwa na kuwasaidia maafisa hao kwa uchunguzi.
Aidha, ameionya wakazi wanaomiliki bunduki kisheria kuzitumia vyema, la sivyo watakabiliwa kisheria huku akiwataka wale wanaomiliki bunduki na bastola kinyume cha sheria kuzirudisha mara moja kabla ya maafisa wa kupambana na ugaidi kaunti ya Mombasa kuwakabili barabara.
"Tayari mshukiwa huyo wa ugaidi anachunguzwa ili kueleza bundiki hizo ametoa wapi na kwa nini anawapa vijana wadogo kuvuruga usalama wa kaunti hii, serikali haitakubali wananchi wasumbuliwe hilo tunawahakikishia wananchi," alisema Marwa.
Wakati uo huo amewataka wakazi kujitokeza waziwazi na kutoa ripoti za washukiwa wa ugaidi kwa maafisa wa polisi ili watiwe nguvuni na kuzuia kushuhudiwa kwa visa vya kihalifu katika kaunti hiyo ya Mombasa.
"Tunawaomba wananchi wajitokeze waziwazi na watuambie wale wanaowashuku kuwa wahalifu na wale wanaoshirikiana na magaidi ili watiwe nguvuni na kuzuia kushuhudiwa kwa visa vya kihalifu katika kaunti yetu," aliongeza Marwa.
Haya yanajiri baada ya mshukiwa wa ugaidi Luqman Khatib Mwashee na Swaleh Mbarak kutiwa nguvuni hivi majuzi na maafisa wa usalama kwa tuhuma za kuhusika na ugaidi pamoja na kuwa wafuasi wa Alshabaab.