Share news tips with us here at Hivisasa

Mshukiwa wa ugaidi Ibrahim Mafud Ashur, atasalia korokoroni kwa siku 21 mpaka uchunguzi kukamilika dhidi ya madai yanayomkabili.

Ibrahimu alitiwa mabaroni mnamo Februari 5, 2016, katika eneo la Malindi kaunti ya Kilifi na kuhusishwa na kundi la Alshabab.

Hii ni baada ya afisa wa upelelezi Fancy Sang’ kuwasilisha ombi la kupewa muda zaidi siku ya Jumatatu, mbele ya hakimu wa Mahakama ya Mombasa Richard Odenyo.

Sang’ aliambia mahakama kuwa anasubiri ripoti kutoka kwa kitengo cha uhalifu jijini Nairobi kinachochunguza simu na tarakilishi za mshukiwa huyo.

Aidha, ameongeza kuwa uchunguzi huo ni wa kina kwani itamlazimu kuchunguza hadi mataifa ya nje kama Sudan na Libya.

Hakimu Richard Odenyo amekubali ombi hilo na kuagiza mshukiwa huyo kuzuiliwa kwa siku 21 katika kituo cha polisi cha Kilindini.

Kesi hiyo itatajwa Februari 29,2016.