Mshukiwa wa ugaidi na mauwaji ya maafisa wa polisi, Ikirima Shosi, ameachiliwa huru baada ya uchunguzi dhidi yake kuonyesha kuwa hausiski na visa vya ugaidi.
Hatua hiyo inajiri baada ya upande wa mashtaka kutaka kumfungulia mashtaka mapya ya kupatikana katika sehemu inayoaminika kuuza dawa za kulevya mnamo Juni 3, 2015 katika eneo la Mwembe Tayari.
Akitoa uamuzi wa kumuondolea mashtaka hayo siku ya Jumanne, Hakimu Richard Odenyo alisema kuwa maafisa wa polisi wamekosa kuwasilisha ushahidi wa kutosha ili kumfungulia mashtaka ya ugadi na kumuhusisha na mashtaka hayo mapya ya ulanguzi wa mihadarati.
Shosi alisalia korokoroni kwa siku 15 tangu kushikwa kwake baada ya afisa ambaye anachunguza kesi hiyo, Peter Munguti, kuwasilisha ombi katika mahakama ya Mombasa la kupewa muda zaidi ili kukamilisha uchunguzi wa kesi hiyo.
Shosi alitiwa mbaroni na mafisa wa polisi mnamo Januari 8,2016, katika mkahawa wa Casablanca kwa tuhuma za kuwa mwanachama wa kundi la al-Shabab.
Alidaiwa kupanga njama za kutekeleza mashambulizi ya kigaidi jijini Mombasa na kuwaficha wanamgambo wa al-Shabab katika nyumba yake iliyoko Guraya.