Mshukiwa wa ugaidi na mauwaji ya maafisa wa polisi Ikirima Shosi atasalia korokoroni kwa siku 15 hadi pale uchunguzi wa madai yanayomkabili utakapotamatika.
Hii ni baada ya afisa anayechunguza kesi hiyo Inpsekta Peter Munguti kuwasilisha ombi la kupewa muda zaidi ili kukamilisha uchunguzi wa kesi hiyo katika mahakama ya Mombasa.
Munguti ameiambia mahakama kuwa anahitaji muda huo ili kuchunguza simu zilizonaswa na mshukiwa huyo pamoja na kuwahoji mashahidi wa kesi hiyo.
Hakimu katika mahakama ya Mombasa Nicolas Njagi amekubali ombi hilo na kuaguza mshukiwa kuzuilwa katika kituo cha polisi cha Kilindini.
Shosi alitiwa mbaroni na mafisa wa polisi siku ya Alhamisi katika mkahawa wa Casablanca kwa tuhuma za kuwa mwanachama wa kundi la Al-shabab, kupanga njama za kutekeleza mashambulizi ya kigaidi jijini Mombasa na kuwaficha magaidi wa Al-shabab katika nyumba yake iliyoko Guraya.
Kesi yake itatajwa Januari 23, 2016 kujuwa iwapo uchunguzi dhidi ya madai yake umekamilika.