Mwanamume mmoja aliponea chupuchupu kuuawa na wakaazi wenye hasira baada ya kufumaniwa akiiba katika duka moja eneo Nguluni kaunti ndogo ya Matungulu usiku was kuamkia Alhamisi.
Akidhibitisha kisa hiki chifu wa kata ya Nguluni Johnbosco Ndambuki alisema kuwa ilikuwa mwendo was saa tao za usiku pale mshukiwa huyu anadaiwa kuvunja na kuingia katika duka hilo alipoanza kubugia pesa mfukoni.
Kelele zake ziliwaamsha wakaazi waliomfumania na kumfungia katika duka hilo kisha kumpa kichapo cha mbwa kabla ya polisi kuwasili.
"Kelele zilizotoka kutokana na mshukiwa huyo kujaribu kuvunja kifuli cha duka hilo iliwaamsha wakaazi waliojifunga kibwebwe kumtia adabu," alielezea Ndambuki.
Chifu ndambuki alielezea kuwa visa vya ukosefu wa usalama vimekuwa mwiba mguuni katika eneo hilo pale maduka huvunjwa kila uchao na bidhaa pamoja na hela kuibiwa.
Mwanamume huyo kwa sasa anatibiwa katika hospitali ya Kangundo level four huku akisubiri kufikishwa kortini haraka iwezekanavyo.
Wakaazi wa eneo hili kwa muda mrefu wamekuwa wakiiomba serikali ya kaunti ya Machakos kuwawekea mataa ya kuhakikisha usalama wakati was usiku juhudi ambazo zimekuwa zikigonga mwamba kila wakati.