Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Polisi katika kaunti ya Kisumu wamemuua kwa kumpiga risasi mshukiwa mmoja wa wizi wa mifugo huku wahalifu wengine wawili wakifanikiwa kutoroka na majeraha ya risasi.

Mshukiwa huyo aliuawa katika eneo la mpaka wa Kaunti za Nandi na Kisumu usiku wa kuamkia siku ya Alhamisi.

Inadaiwa kuwa mshukiwa huyo kwa jina Willy Kabur, alikuwa amejihami kwa bunduki, huku wenzake wawili wakidaiwa kujihami kwa mishale.

Polisi waliwashambulia washukiwa hao kwa risasi, baada yao kudaiwa kuanza kuwakabili polisi waliokuwa wakishika doria.

Kwenye kikao na wanahabari jijini Kisumu, Kamanda wa polisi katika jimbo la Kisumu Joseph Keitany alisema kuwa Kabur ashawahi kufungwa na kutoroka jela kutokana na tuhuma za za wizi wa mifugo.

“Washirika wa marehemu wana mda wa saa 24 kujasalimisha, la sivyo polisi wawaandame,” akaonya Keitany.

Mwili wa mwendazake unahifadhiwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga almaarufu Russia jijini Kisumu.

Hali ya wasi wasi na mapigano vimeshuhudiwa katika eneo la Kibigori kwenye mpaka wa Kaunti za Kisumu na Nandi katika siku za hivi maajuzi, kutokana na kukithiri kwa visa vya wizi wa mifugo.