Huku matokeo ya mtihani wa darasa la nane yakitarajiwa kutangazwa siku ya Jumatano, mfungwa katika gereza la Shimo la Tewa, Mary Wangechi, mwenye umri wa miaka 25 ameelezea matumaini yake ya kupata zaidi ya alama 380 katika mtihani huo.
Wangechi, ambaye anatumikia kifungo cha miaka mitano gerezani, ni miongoni mwa wasichana wanne waliokalia mtihani huo katika gereza hilo mwezi Novemba mwaka huu.
Ameeleza kuwa alilazimika kurudilia masomo yake gerezani baada ya kuacha masomo katika kidato cha pili kutokana na changamoto za kifedha, hivyo basi kutumia fursa hiyo gerezani ili kujiendeleza kimasomo.
Kwa sasa Wangechi anasema kuwa yuko tayari kuendelea na masomo ya sekondari endapo atafaulu katika mtihani wa KCPE na kupata ufadhili, akisema kuwa alilazimika kurudia masomo ya darasa la nane kutokana na kutokuwepo kwa masomo ya sekondari katika gereza hilo upande wa wanawake ambapo ni mwanafunzi mmoja anayejisomea wa kidato cha kwanza.