Katibu wa serikali ya Kaunti ya Nyamira Erick Onchana amelazimika kumuachisha kazi kwa muda msimamizi wa wafanyikazi kwenye kaunti hiyo, Prof Kennedy Ongaga.
Haya yanajiri baada ya Ongaga kushtakiwa kwa tuhuma za uharibifu wa mali ya nduguye wiki jana kwenye mahakama ya Nyamira.
Kwenye kikao na wanahabari afisini mwake siku ya Jumatatu, Onchana alisema alilazimika kuchukua hatua hiyo kwa mujibu wa sheria kwa kuwa afisa yeyote aliye na kesi mahakamani sharti asimamishwe kazi hadi pale kesi inayomkabili itakaposikizwa na kuamuliwa.
"Kulingana na sheria za Kenya, afisa yeyote aliye na kesi mahakamani sharti aachishwe kazi kwa muda hadi pale kesi yake itakaposikizwa nakuamuliwa, hali ambayo imenilazimu kumsimamisha kazi kiongozi wa wafanyikazi Prof Ongaga," alisema Onchana.
Onchana aidha aliwapa changamoto wafanyikazi wengine wa serikali kuwa na maadili mema na kutafuta mbinu yakusuluhisha tofauti baina yao na familia zao, badala yakulumbana na kisha kujihusisha na uharibifu wa mali ya watu wengine.
"Kama wafanyikazi wa serikali, sharti tuonyeshe mfano mwema kwa wale tunao waongoza badala yakujihuzisha na visa ambavyo vinaweza kutuharibia jina kwa wananchi,” alisema Onchana.
Ongaga alikuwa amefikishwa kwenye mahakama ya Nyamira kwa shtaka la kuharibu mali ya mke wa nduguye yenye thamani ya Sh200,000 na kuachiliwa kwa dhamama ya Sh0,000 na mdhamini wa kiasi sawa.