Share news tips with us here at Hivisasa

Mkurugenzi wa sekta ya afya katika kaunti ya Kisii Geoffrey Ontomu amewahimiza wakaazi katika kaunti hiyo kutowabagua na kuwatenga wanaoishi na virusi vya ugonjwa wa Ukimwi katika jamii.

Wito huo umetolewa baada ya uchunguzi kuonyesha kuwa idadi nyingi ya wagonjwa hao hupoteza maisha yao wanapotengwa na kubaguliwa katika jamii jambo ambalo huwapelekea wengi wao kuwa na msongo kisha kufariki.

Ontomu alisema wanaoishi na virusi vya Ukimwi wana uwezo wa kuishi kama wakaazi wengine wa kawaida katika jamii na hakuna haja ya kutengwa katika jamii.

Ontomu aliomba wazazi kuwapeleka shuleni watoto wao ambao wameathirika na ugonjwa huo kwani watasoma na kuwa kama wengine

“Hakuna haja kwa wakaazi kubagua wale wanaoishi na Ukimwi maana wako kama watu wengine na watu hao wanapobaguliwa mara nyingi huwa wanafariki kutokana na misongo,” alisema Ontomu.

“Wale watoto walio na virusi hivyo vya ukimwi naomba wasomeshwe kwani watakapomaliza shule wataweza kusaidia wazazi,” aliongeza Ontomu.