Afisa mkuu wa gereza la Nakuru GK James Sawe amedai kuwa msongamano katika gereza hilo umesababisha ongezeko la visa vya ugonjwa wa kifua kikuu.
Akizungumza na wanahabari Jumanne katika gereza hilo, Sawe alisema gereza hilo linafaa kuwa na wafungwa na wale walio rumande 700, lakini kwa sasa ina jumla ya watu 1,562.
Hata hivyo, amedhibitisha kuwa maafisa wa kitengo cha afya kwenye gereza hilo wanafanya kila wawezalo kuhakikisha kuwa wafungwa wote na walio rumande wanachunguzwa ili kubaini iwapo wana ugonjwa huo.
Wakati huo huo, afisa huyo amehoji kuwa wengi wa walio chini ya kifungo cha rumande wanatoka mjini Molo na kutokana na hilo, ameitaka serikali kuweka mikakati ya ujenzi gereza mjini humo.
Kwa upande wake, afisa wa kitengo cha afya kwenye gereza hilo ambaye pia alizungumza na wanahabari kwa jina la Julia Miring’u alisema kuanzia mwezi Septemba, kumeripotiwa visa 25 yva ugonjwa wa kifua kikuu.
Kulingana naye, wanaochunguzwa na kubainika kuwa wana ugonjwa huo huwekwa chini ya uangalizi wa maafisa wa afya kwenye wadi spesheli iliyo katika gereza hilo .
Ni hatua anayosema huzuia maambukizi mapya ya ugonjwa huo kwenye gereza hilo, ikizingatiwa kuwa kuna msongamano mkubwa.