Mkurugenzi mkuu wa Tume ya kudhibiti kawi nchini ERC mhandisi Joe Ng’an’ga amesema kuwa kuna mswada utakaowasilishwa bungeni kuhakikisha kuwa wanaopatikana na makosa ya kuwauzia Wakenya mafuta ya petroli yaliyochanganywa na yale ya taa wanaadhibiwa vikali.
Katika kikao na wanahabari siku ya Jumatano kwenye hoteli ya Merica mjini Nakuru, mkurugenzi huyo alisema kuwa mswada huo unapendekeza faini ya chini zaidi (minimum fines) ambayo inaweza kutozwa anayepatikana na kosa hilo badala ya adhabu iliyopo kwa sasa ambayo inaangazia tu faini ya juu zaidi (maximum fines) ambayo mtu huyo anaweza kutozwa.
Ng’an’ga alisema adhabu iliyopo kwa sasa kwa anayepatikana na kosa hilo inaonyesha kuwa anayepatikana na kosa hilo hawezi kutozwa faini inayozidi shilingi milioni moja, hatua anayosema inaweza kupelekea mahakama kumtoza faini ya chini anayepatikana na kosa hilo.
Ni adhabu ambayo pia alisema imepelekea baadhi ya vituo vya mafuta kuendelea na tabia hiyo, ikizingatiwa kuwa wanapata fedha nyingi kutokana na biashara hiyo ikilinganishwa na adhabu wanayotozwa ambayo ni ndogo sana kwao.
Wakati huo huo, mkurugenzi huyo alisema kuwa mshauri wao amekuwa akizuru vituo mbalimbali vya mafuta hapa nchini huku akichukua sampuli za mafuta yanayouzwa kwenye vituo hivyo, lengo likiwa kufanya uchunguzi wa kubaini iwapo mafuta yanayouzwa ni yale yanayofaa au ikiwa yamechanganywa na mafuta ya taa au dizeli.
Hata hivyo, Ng’ang’a amesisitiza kwamba shughuli hiyo inaendelezwa kwa siri na kuwa miji au vituo atakavyozuru haviwezi kuwekwa wazi kwani wanaomiliki vituo hivyo huenda wakavifunga katika harakati za kuzuia kupatikana na hatia hiyo.