Kinara wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, amesema yeye ndiye ‘maji ya kuzima joto la Jubilee na Cord’, na aidha mwaniaji bora wa kuingia ikulu.
Akizungumza mjini Molo kaunti ya Nakuru Jumapili, Mudavadi alisema atatoa uongozi mbadala, tofauti na ule wa Jubilee ama CORD, huku akitupilia mbali madai kwamba amejiunga na miungano hiyo, kama inavyoelezwa na baadhi ya wabunge kutoka Magharibi kwamba makubaliano aliyotia saini yanamfanya aunge mkono Jubilee.
"Ninawezaje kusaidia watu ambao ni wacheshi, mimi sio kiongozi wa UDF, naongoza ANC ambacho ni chama cha kipekee," alisema Mudavadi.
Mudavadi alisema hayo wakati wa mazishi ya ndugu shemejiye, katika eneo la Kamure kaunti ndogo ya Molo.
Alikanusha kutia saini mkataba wowote na chama cha Jubilee, akisema maelewano hayo yalikuwa chini ya vyama vya Amani na Jubilee ambavyo sasa havimo.
Mudavadi alisema uvumi wa wabunge wa UDF akiwemo Emmanuel Wangwe wa eneo bunge la Navokholo, Benjamin Washiali anayewakilisha Mumias Mashariki, na Bernard Shinali wa Ikolomani hayana msingi na yanalenga kuvuta vyuma azma yake ya kupigania urais uchaguzi mkuu ufikapo.
Wabunge hao walidai kwamba Mudavadi alijiunga na chama cha Jubilee baada yake kutia saini makubaliano ya baada ya uchaguzi wakati alikuwa kiongozi wa UDF.