Shirika la kutetea haki za binadamu la Muhuri linaitaka serikali kuliondoa jeshi la KDF nchini Somalia kwa kile limekitaja kama hatua itakayoleta suluhu ya kudumu kwa vita vya mara kwa mara baina ya majeshi ya Kenya na wanamgambo wa Al Shabaab.
Kwenye kikao na wanahabari afisini mwake mjini Mombasa siku ya Jumatatu, mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Hassan Abdille, alihimiza serikali kuwaondoa wanajeshi hao nchini Somalia, na badala yake kuwapeleka katika boda ya Kenya ili waimarishe usalama wa nchi.
''Ili kukomeza vita dhidi ya Al Shabaab, lazima majeshi yetu yatoke Somalia, hakuna haja wasalie kule na huku pia tunaishi kwa hofu,'' alisema Abdille.
Abdille aliutaja uwepo wa wanajeshi wa Kenya nchini Somalia kama chanzo cha vita vya mara kwa mara baina ya wanajeshi hao na wanamgambo wa Al Shabaab.
Mtetezi huyo wa haki za binadamu vilevile alituma risala za rambi rambi kwa familia ambazo zilipoteza jamaa yao katika shambulizi lililotekelewa na Al Shabaab katika kambi ya majeshi ya muungano wa Afrika nchini Somalia Ijumaa iliyopita.
Aidha, aliitaka serikali kuzifidia familia hizo.