Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa Kilifi Kaskazini Gideon Mung’aro amekubali kushindwa kwa aliyekuwa mgombea wa kiti cha eneo bunge la Malindi kwa tiketi ya chama cha Jubilee Philip Charo, katika uchaguzi mdogo uliofanyika siku ya Jumatatu.

Akizungumza na wenyeji mjini Malindi siku ya Jumanne, Mung’aro, ambaye ni mbunge hasi wa muungano wa Cord alisema kuwa anayaheshima maamuzi ya wakazi wa Malindi, lakini atahakikisha kuwa Mkoa wa Pwani unajiunga kikamilifu na chama kipya cha JAP katika uchaguzi mkuu ujao.

"Wakazi wa Malindi wamezungumza, kwa hivyo tumekubali. Lengo langu sasa ni kuhakikisha kuwa Pwani kwa jumla katika uchaguzi ujao unakuwa ndani ya serikali kwa kukipigia kura chama cha JAP,’’ alisema Mung’aro.

Aidha, aliwahakikishia wakazi kuwa ahadi zote walizotoa wakati wa kampeni zitatimizwa licha ya mwaniaji waliompigia debe katika uchaguzi huo kushindwa.

"Nitazungumza na Rais Kenyatta, atakuja hapa kuitekeleza miradi aliyoahidi kuwafanyia wakazi wa Malindi,’’ aliongeza Mung’aro.

Kwa upande wake Philip Charo, aliyepoteza katika uchaguzi huo, alimtakia mema mshindani wake Willy Mtengo na kuapa kushirikiana na wakazi katika harakati za kuiendeleza miradi ya maendeleo.

Willy Baraka Mtengo wa ODM alichaguliwa mbunge mpya wa eneo bunge la Malindi baada ya kuzoa kura 15,406 na kumshinda Philip Charo wa Jubilee aliyepata kura 9,064 katika uchaguzi mdogo uliofanyika siku ya Jumatatu.

Picha: Mbunge wa Kilifi Kaskazini Gideon Mung’aro. Amekubali kushindwa kwa aliyekuwa mgombea wa kiti cha eneo bunge la Malindi kwa tiketi ya chama cha Jubilee Philip Charo. Maktaba