Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Kilifi, Aisha Jumwa, amemtaka mbunge wa Kilifi Kaskazini Gideon Mung’aro kutangaza rasmi kukihama chama cha ODM, badala ya kuziuza sera za mrengo wa Jubilee, huku angali mbunge wa chama hicho.
Jumwa alimtaja Mung’aro kama msaliti, na kumtaka kujiondoa kwenye chama hicho, ili kutoa nafasi kwa uchaguzi mdogo kufanywa katika eneo bunge lake.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano katika uzinduzi wa barabara ya Fidel Odinga iliyohudhuriwa na kinara wa Cord Raila Odinga, Jumwa alimtaka Mung’aro kukoma kulitumia jina la chama hicho katika kampeni zake na badala yake kujitangaza kama mbunge wa Jubilee.
“Ikiwa anajiamini, akihame chama cha ODM halafu akiwanie tena kiti hicho kwa tiketi ya chama cha Jubilee, tuone kama kweli yeye ni mwanaume halisi,” alisema Jumwa.
Kauli ya Jumwa inajiri siku mbili tu baada ya Mung’aro kuwasuta wakosoaji wake na kuapa kukipigia debe chama kipya cha JAP, huku akiwaonya viongozi wa ODM kuwa atawashtaki kortini ikiwa watajaribu kumuondoa chamani.
Mung’aro ni miongoni mwa baadhi ya wanasiasa kutoka eneo la Pwani, ambao tayari wametangaza kukihama chama cha ODM na kujiunga na mrengo wa Jubilee, hatua ambayo inazidi kuibua joto la siasa katika eneo hilo.