Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa Kilifi Kaskazini Gideon Mung’aro amekuwa kiongozi wa hivi punde kuwahimiza viongozi wa eneo la Pwani kujiunga na muungano wa Jubilee katika uchaguzi wa 2017 ili kuhakikisha kuwa mkoa huo unakuwa ndani ya serikali ijayo.

Akizungumza muda mchache baada ya kuhitimu na cheti cha digrii katika chuo kikuu cha Gretsa, Mung’aro alisema kuwa muda umewadia kwa eneo la Pwani kuwa ndani ya serikali.

‘’Hatuwezi kuwa katika upande wa upinzani tena, lazima tuhakikishe kuwa watu wetu wanawakilishwa serikalini ili nasi tufaidi wakati wa mgao wa uongozi nchini,’’ alisema Mung’aro.

Mung’aro, ambaye alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha ODM katika uchaguzi wa 2013, alitumuliwa na muungano wa Cord kama kiongozi wa wachache bungeni baada ya kuibuka madai kuwa alikuwa akihujumu upinzani kwa kufanya kazi na serikali.

Kauli ya mbunge huyo inajiri siku chache tu baada ya pendekezo kama hilo kutolewa na baadhi ya wabunge wa eneo la Pwani wanaounga mkono muungano wa Jubilee katika mkutano wa kisiasa wikendi iliyopita.