Muundo wa barabara ya Salgaa unafaa kurekebishwa ili kupunguza visa vya ajali katika eneo hilo, ambavyo vimeongezeka siku baada ya nyingine.
Akizungumza Jumatatu katika eneo hilo la Salgaa, mwenyekiti wa shirika la kupambana na dawa za kulevya na mihadarati nchini John Mututho alisema muundo wa barabara hiyo ndio chanzo cha ajali nyingi ambazo hutokea.
Ameitaka idara inayoshughulikia barabara nchini kuutathmini muundo wa barabara hiyo na kuurekebisha ili kuzuia ajali zinazotokea eneo hilo kila mara.
Hii ni baada ya watu wanane kufariki kwenye barabara hiyo katika visa viwili vya ajali mwishoni mwa wiki jana, wakiwemo vijana waliofariki wakati wa mkesha wa kuamkia mwaka mpya.
Kwa habari husika, watu 32 wamefariki kutokana na ajali za barabarani mwaka huu.
Francis Mejja, ambaye ni mkurugenzi kutoka mamlaka ya usalama barabarani amesema idadi ya waliojeruhiwa imeongezeka kutoka 80 hadi zaidi ya watu 200 katika kipindi kama hicho mwaka jana wa 2015.