Share news tips with us here at Hivisasa

Muungano wa mawaziri wa kaunti 47 nchini wameishutumu tume ya mishahara na marupurupu ya wafanyikazi wa umma nchini kwa kuwakandamiza mawaziri hao kulingana na viwango vya kikazi.

Kulingana na Mwenyekiti wa Muungano huo Antony Njaramba, Tume hiyo imeonekana kuwakandamiza mawaziri hao kwa muda wa miaka mitatu sasa, licha ya viongozi wa muungano huo kuiandikia barua ya kuwepo kwa vikao vya mazungumzo ili kujadili kusawazishwa wa mishahara.

Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Njaramba ambaye pia ni Waziri wa Kilimo kaunti ya Mombasa, amesema kwamba kamwe mawaziri hao hawajataka kuongezwa mshahara jinsi tume hiyo inavyosema, bali wanapendekeza kuwepo kwa usawa wa mishahara na ugavi wa marupurupu.

Njaramba amezidi kuikosoa tume hiyo akisema kwamba itaangamiza taifa hili iwapo hawatatatua mzozo ya misharaha ya Wafanyikazi wa umma kwa njia mwafaka, huku akiwataka makamishna wa tume hiyo kutenga siku rasmi ya kufanya vikao vya mazungumzo na viongozi wa mawaziri hao.

"Sisi kama mawaziri wa kaunti 47 nchini hatujasema kwamba tunahitaji kuongezwa mishahara kama vile makamishna wa tume ya SRC wanavyosema, sisi tunataka kuwepo na usawa wa ugavi wa marupurupu na mishahara kulingana na vitengo mbalimbali vya kazi," alisema Njaramba.

Haya yamejiri baada ya tume ya SRC kutowatengea mawaziri hao marupurupu yao kulingana na vitengo vyao vya kazi ilikilinganishwa na wafanyikazi wa umma huku mawaziri wengine wa kaunti wakipata marupurupu ya chini zaidi.