Muungano wa mawaziri wa kaunti umejitenga na madai kuwa wanataka kuongezewa mishahara, na kusema kuwa Jumuia hiyo inataka usawa katika marupurupu yanayopewa wafanyakazi wa umma kuwa wa viwango sawa kama wengine.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kupitia kwa mwenyekiti wa Jumuia hiyo Anthony Njaramba, ambaye alikuwa akiwahutubia waandishi wa habari siku ya Jumatatu katika Kaunti ya Mombasa, alisema kuwa zile hela wanapata kama marupurupu si sawa, na akapendekeza kuwa tume ya kusimamia mishahara na marupurupu ya wafanyakazi wa umma, SRC, kuliangalia suala hilo ili kuwekwa sawa.

Njaramba ambaye ni waziri wa kilimo kwenye Kaunti ya Mombasa alisema kuwa inakuwa utata wakati tume ya mishara na marupurupu inapowapa marupurupu maafisaa wengine na mawaziri kukosa.

“SRC inahitaji kusawazisha marupurupu ya afisa wa umma, si sawa unapopata dereva anapewa marupurupu ya kuongea kwenye simu na mawaziri hawapewi,” alisema Njaramba.

Kiongozi huyo alishangaa ni kwa nini wasipewe marupurupu ambayo yanasawiana na kazi ambayo wanatekeleza, ikizingatiwa kuwa baadhi ya maafisa wa idara nyingine za umma wamepewa marupurupu yao.

Tume ya kusimamia mishahara na marupurupu ya wafanyakazi wa umma imekuwa ikijipata katika malumbano na wafanyakazi wa idara mbalimbali za umma kwa suala la mishahara na marupurupu, ya karibuni zaidi yakiwa ya madaktari na walimu ambao wamekuwa katika migomo na bado masuala kama ya walimu hayajapata suluhu la kuridhisha.