Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Muungano wa Kiuchumi baina ya Kaunti za North Rift utakabiliana na visa vya wizi wa mifugo miongoni mwa jamii za Wapokot na Waturkana.

Gavana wa Kaunti ya West Pokot Bw Simon Kachapin alisema muungano huo ambao unalenga kuboresha uchumi wa kaunti wanachama utakuwa nguzo muhimu ya kukabiliana na wizi wa mifugo.

Bw Kachapin alisema wizi huo umekuwa ukichangiwa mara kwa mara na umaskini miongoni mwa wakazi wa kaunti husika.

Akihutubu mjini Eldoret siku ya Jumanne, Bw Kachapin alisema iwapo muungano huo al maarufu Noreb utazingatia mapendekezo ya kila kaunti kuhusu vigezo muhimu vya kuboresha uchumi, bila shaka kaunti ambazo ziko katika maeneo kame zitaboresha uchumi wake na kuzika katika kaburi la sahau tamaduni ya wizi wa mifugo.

“Changamoto ya wizi wa mifugo na uhasama kati ya jamii za Wapokot na Waturkana ni mojawapo ya maswala ambayo yamekuwa yakirudisha nyuma uchumi wetu tangu utawala wa kaunti uanze kushika kasi,” alisema Bw Kachapin.

Gavana Kachapin alisema wizi wa mifugo na uhasama baina ya jamii husika hutokana na umaskini na kutengwa kimaendeleo.

“Nina imani Noreb itaboresha uchumi wa jamii zetu ambapo vijana watakuwa na shughuli bora na halali za kuboresha maisha yao hivyo basi hakutakuwa na wakati wa kushiriki katika tamaduni duni ya uwizi wa mifugo inayotoa taswira mbaya kwa wananchi wetu.”

Wiki jana mji wa Eldoret, Noreb uliandaa kongamano la siku tatu kuhusu uwekezaji baina ya kaunti wanachama.