Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika kautni ya Nakuru imeathiri pakubwa kilimo cha nyanya katika maeneo mengi yanayotegemea kilimo hicho.

Katika utafiti uliofanywa na mwandishi huyu imebainika kuwa wakulima wengi wa nyanya katika eneo buneg la Subukia wamelazimika kupanda viazi baada ya mvua kuzidi na kuharibu mimea ya nyanya.

Baadhi ya wakulima wameeleza kuwa walilazimika kuasi kilimo cha nyanya baada ya kubainika kuwa watapata hasara kutokana na kuoza kwa bidhaa hiyo.

John Ngige ambaye awali alikuwa akilima nyanya alisema kuwa mvua kubwa huathiri uzalishaji nyanya na pia bei yake hupungua kutokana na hali mbovu ya mazao.

“Wakati wa mvua ni vigumu kukuza nyanya kwa sababu mazao hurudi chini na nyanya huoza hata kama bado zingali shambani na ndio sababu wengi wa wakulima wameamua kulima viazi kwa sababu hivyo vitakaa chini ya ardhi na haviwezi kuharibiwa na mvua vikiwa mchangani,” akasema.

“Tena mvua ikiwa kubwa magonjwa ya nyanya huwa mengi na hapo utapata bei pia inapungua na unapata hasara kama mkulima kwa sababu hata kupuliza dawa kwenye mimea wakati wa mvua si vizuri,” akaongezea.

Mary Mwangi ambaye pia alikuwa akilima nyanya alisema alilazimika kubadili nia baada ya mvua ya elnino kuanza na kuharibu shamba lake la nyanya.

“Nilikuwa nimepanda nyanya lakini mvua ilikuja ikaharibu na nikaamua kupanda viazi amabavyo naamini vina faida kuliko nyanya,” akasema.

Eneo la Subukia ya chini nio baadhi ya maeneo yanayoshuhudia mafuriko kutokana na kufurika kwa mito katika maeneo hayo.