Mbunge wa Likoni Mwalimu Masoud amemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuwaondolea gharama ya shilingi elfu 182 wakazi wa Shamba la Waitiki kama ilivyoagiza serikali hapo awali.
Mwahimu amesema kuwa wakazi wa eneo hilo hawana fedha za kulipa gharama hiyo, na iwapo swala hilo litaangaziwa, basi itakuwa afueni kwa wakazi hao.
Akizungumza katika eneo la Shika Adabu huko Likoni mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Mwahima alimtaka Rais Uhuru kuhakikisha pia kivuko cha Mtongwe kinaboreshwa ili kupunguza msongamano katika kivuko cha feri cha Likoni.
"Tunakuomba mheshimiwa rais kuturejeshea feri ya Mtongwe ili kurahisisha shughuli za uchukuzi na kupunguza msongamano wa kivuko cha feri cha Likoni," alisema Mwahima.
Naye mbunge wa Kisauni Rashid Bedzimba ameunga mkono swala hilo, huku akipendekeza kujengwa kwa daraja jipya katika eneo la kivuko cha feri ili kupunguza msongamano na kurahisisha shughuli za uchukuzi na utalii.
Kwa upande wake mbunge wa Mvita Abdulswamad Sharrif Nassir amesema kuwa swala hilo litasaidia wakazi hao, japo akipendekeza serikali kuwaruhusu wavuvi 1,700 wa kaunti hiyo kuvua samaki eneo linalotumiwa na wachimbaji mchanga wa reli ya kisasa.