Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mbunge wa Likoni mwalimu Masoud Mwahima amewataka wakazi wa eneo bunge hilo kutolaghaiwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa na kuikosoa miradi ya serikali ikiwemo suala la ardhi, akisema kuwa serikali imejitolea kuwasaidia Wakenya.

Akiongea na wanahabari katika eneo bunge lake la Likoni, Mwahima amesema kuwa shughuli ya utaoaji wa hati miliki za ardhi zilizosalia unaendelea kutekelezwa ili kuhakikisha kuwa kila familia inapata hati miliki.

Mwahima amewataka wakazi wa Likoni kuwa katika mstari wa mbele kufanya kazi na serikali ili kuona kwamba miradi ya kimaendeleo inatekelezwa katika eneo bunge hilo na kuwafaidi wakazi wa Likoni.

Wakati uo huo amewasuta viongozi wanaomkejeli Rais Kenyatta na kusema kuwa Rais wa taifa hili hawezi kuwekewa mipaka ya kuzuru eneo analotaka kwani ni kiongozi wa taifa lote na akawakosoa wanaodai kuwa mradi wa taa mtaani katika kaunti hiyo ni mradi wa serikali ya kaunti ya Mombasa.

"Nataka kuwaambia viongozi wa kisiasa msijaribu kumkejili Rais wa Kenya kwa sababu ni kiongozi wa taifa zima na sisi kama wakaazi wa Likoni tutaendelea kufanya kazi na serikali ili kufanikisha miradi ya kimaendeleo mashinani," alisema Mwahima.

Mbunge huyo wa Likoni amewahimiza wakazi wa eneo bunge lake kushirikiana kwa karibu mno na serikali kuu ili kufaidi na mradi ya kimaendeleo mashinani.