Mwakilishi wa Wadi ya Kongewea Jabes Oduor amemtetea Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho, dhidi ya shtuma za kutowajibika kazini.
Haya yanajiri baada ya kuzuka madai kuwa gavana huyo anasita kutia sahihi baadhi ya miswada inayopitishwa na bunge la kaunti hiyo.
Kwa mujibu wa tarakimu za kaunti kuhusu miswada inayojadiliwa na bunge za kaunti, bunge la Kaunti ya Mombasa chini ya miaka miwili iliyopita limejadili miswada 41 ambapo 17 ndizo zimepitishwa.
Licha ya hayo, inadaiwa kuwa Gavana Joho ametia sahihi kuwa sheria mswada mmoja pekee, jambo ambalo limeibua hisia kinzani kuhusu uwajibikaji wa kiongozi huyo.
Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa gazeti la the Star siku ya Jumanne, mwakilishi Oduor alisema hakuna sheria inayomlazimu gavana kutia sahihi kila mswada unaopitishwa na bunge kuwa sharia, hivyo Joho hafai kulaumiwa.
“Gavana ana uhuru wa kuchagua ni mswada upi unaofaa kuwa sheria baada ya kushahuriana na mawakili wake, hivyo tusimlaumu kiongozi wetu,” alisema Jabes.
Bunge la Kaunti ya Mombasa siku ya Jumanne lilipitisha mswada utakaowezesha barabara zote za mji kuwa chini ya usimamizi wake na wala sio serikali kuu kama ilivyokuwa hapo awali.