Mwakilishi wa wadi ya Port Reitz, Fadhili Mwalimu, ametetea mswada wa kutaka wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa TUM, waadhibiwe kwa kuharibu mali waliposhiriki mgomo, kwa kusema kuwa mswada huo unalenga kulainisha mawazo na fikira potovu za wanafunzi kwa jumla.
Akizungumza kwenye mahojiano katika ofisi za bunge la Kaunti ya Mombasa siku ya Jumatutu baada ya kikao na viongozi wa wanafunzi wa chuo hicho, Mwalimu alisema kuwa ili kupunguza visa vya ghasia ambazo hushuhudiwa miongoni mwa wanafunzi wa vyuo mbalimbali kwenye Kaunti, sharti sheria iwekwe ili kuwaongoza.
Bwana Mwalimu, alisema kuwa vijana hasa wale walio katika taasisi pamoja na vyuo vikuu wana mazoea ya kuharibu mali wanapogoma, kwa kuchoma na kupora bidhaa za watu wanaoendesha biashara zao karibu na wanakofanyia ghasia hizo.
“Kupitishwa kuwa mswada kama huo utakuwa dawa ya kuzuia visa vya mara kwa mara vya wanafunzi kuzua ghasia na kuharibu mali wanapotofautiana na vyuo na taasisi husika,” alisema Mwalimu.
Aliongeza: “Si chuo cha TUM tu kinalengwa na mswada huu ila ni kila chuo kilichoko katika Kaunti ya Mombasa. Mswada huu unalenga kuwa kielelezo kwa wale wanafunzi ambao watakuwa na nia mbaya ya kuzua fujo.”