Mwakilishi mteule wa bunge la kaunti ya Nyamira Naomi Ondieki amelalamikia vikali kutupwa kwa takakataka kando kando mwa barabara za mji wa Nyamira. 

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akiongea na wanahabari nje ya majengo ya bunge la kaunti ya Nyamira Ijumaa, Ondieki alihoji kuwa hali hiyo ya taka kutupwa kila mahali babarani ni tishio kwa wananchi kwa kuwa huenda ikasababisha magonjwa mbalimbali kama vile kipindupindu. 

"Takataka ambazo hutupwa ovyo kando kando mwa barabara ni tishio kwa wananchi, hasa wachuuzi na wanunuzi wa vyakula vinavyopikwa kando kando mwa barabara kwa maana huenda taka hizo zikawasababishia magonjwa," alisema Ondieki. 

Aliongeza kwa kusema kuwa kamati ya kawi, mazingira, maji na raslimali kwenye bunge la kaunti ya Nyamira inafaa kushughulikia swala hilo kwa dharura ili kuhakikisha kuwa hali hiyo imerekebishwa. 

"Kamati ya kawi na mazingira yafaa kushughulikia swala hilo kwa dharura ili kuhakikisha kuwa taka hizo zinaondolewa kwenye sehemu hizo kwa haraka ili kuhakikisha kuwa maisha ya wakazi hayaathiriki kivyovyote," alihoji Ondieki.

Akizungumzia swala la kutafuta mahala pa kutupwa takataka, Ondieki ameiomba serikali ya kaunti kuweka mikakati ya kununua ardhi ambayo itasaidia pakubwa kuweka takataka. 

"Namwomba gavana Nyagarama aweke mikakati yakuhakikisha kuwa ardhi imenunuliwa ili itumiwe kutupia takataka kwa kuwa hali ya kutupwa takataka hizo barabarani zinasababisha uchafuzi wa mazingira," aliomba Ondieki.