Akina mama ambao waume zao waliohusika katika vita vya mauamua kutoka eneo la Gilgil, Kaunti ya Nakuru wametoa wito kwa serikali kuwakumbuka na kuwatengea fedha za kuwafidia hasaa wakati huu wa uzeeni.
Wakiwakilishwa na mmoja wao kwa jina la Wanjiku Ng’ang’a aliyekuwa akizugumza kwenye mkutano wa akina mama uliokuwa umeandaliwa Ijumaana mwakilishi wa akina mama katika Kaunti ya Nakuru Mary Njoki Mbugua, akina mama hao walielezea shida ambazo wamekuwa wakipitia tangu kuachwa na waume wao waliofariki wakipiginia uhuru wa nchi hii.
"Kuna akina mama ambao waume wao waliaga wakati wa vita vya maumau. Akina mama hao hawana hata ploti wanayoweza kupanda vyakula. Hawana nyumba zao bali inawabidi kukodisha. Itakuwa vyema ikiwa wanaweza kupata ploti ya kujenga nyumba," alisema Wanjiku.
Kwa upande wake, mwakilishi wa akina mama katika Kaunti ya Nakuru Mary Mbugua amewahakikishia akina mama hao kuwa maswala yao yataangaziwa, akielezea kuwa analenga kuwasilisha mswada kwenye bunge wa kuwasaidia akina mama wanaowalea watoto wao bila ya usaidizi wa waume zao.
"Kuna mswada ambao tayari nimeandika. Nitapanga kuuwasilisha bunge na tayari ninazungumza na mawakili ili tuone mswada huo utakuwa vipi. Mswada huo ni wa wajane na akina mama wanaowalea Watoto wao bila ya usaidizi wa waume zao," aliashiria mwakilishi huyo wa Wanawake.
Aidha Mbugua ameelezea furaha yake ya uamuzi wa mahakama wa Alhamisi ya tarehe 21 Januari wa kuagiza kuwachiliwa kwa shilingi bilioni mbili za akina mama, huku akitarajia kuwa zilizosalia zitatolewa kwa muda usiokuwa mrefu ili kuwafaa akina mama.