Mwakilishi wadi ya Gesima Ken Atuti amejitokeza kutangaza wazi kwamba tayari ametenga shillingi millioni 100 ili kumaliza ujenzi wa kituo cha mafunzo kule Gesima, ujenzi ambao kwa muda umekuwa ukisimama baada ya hazina ya maendeleo bunge kusitisha ujenzi wake.
Akihutibu kule Gesima siku ya Jumapili, Atuti alisema kuwa usitishaji wa mradi huo ni hatua ya kughadhabisha, huku akihoji kuwa alilazimika kuchukua hatua hiyo ili kuwawezesha wakazi wa eneo hilo hasa vijana kupata nafasi ya kupata elimu.
"Ni jambo la kughadhabisha kuwa mradi huu wa ujenzi wa kituo hiki ulisitishwa na nimeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa nimetenga shilllingi millioni 100 kwa minajili ya kumaliza ujenzi wa kituo hiki na hilo litawezekana pindi tu serikali itakapotupa pesa za ustawishaji maendeleo wodi," alisema Atuti.
Atuti aidha aliwapa changamoto walimu kuhakikisha kuwa kituo hicho kinatumiwa kwa manufaa ya wakazi wa eneo hilo huku akiwahimiza viongozi wa kisiasa katika eneo hilo kuweka mikakati ya kuhakikisha vituo sawia na hivyo vinajengwa ili kuwasaidia wenyeji.
"Nawapa changamoto walimu kuhakikisha kuwa kituo hiki kinawanufaisha wenyeji na kwa kuwa tunahitaji vituo vingi kama hivi ni ombi langu kwa viongozi wa eneo hili kuhakikisha kuwa vituo vingi vya elimu vinajengwa katika eneo," aliongezea Atuti.