Mwakilishi wa Wadi ya Biashara katika eneo bunge la Ruiru Bwana Joseph Matuga ameahidi kuendeleza vita dhidi ya dawa za kulevya, kuleta maendeleo na elimu ya vijana katika eneo lake.
Akizungumza kwenye hafla ya vijana siku ya Jumatatu katika uwanja wa Kanisa ya Ruiru PCEA, Matuga alisema kuwa vijana wana nafasi murua ya kuelimisha na kuikukuza jamii kulingana na hali ya uchumi.
Matuga alisisitiza kuwa lazima vijana wawe na uwezo wa kutambua lililo zuri na bovu ili waweze kuweka kielelezo chema kwa vizazi vijavyo.
Mwakilishi huyo alisema kuwa yu tayari kushirikiana na yeyote ambaye ana wazo la kujikuza na kuikuza jamii iliyokaribu naye.
Alisema kuwa hatoshirikiana na yeyote ambaye anendeleza biashara ya ulanguzi wa dawa za kulevya wala hatoshirikiana na yeyote ambaye yuauzia wakazi pombe haramu.
Aliendelea kwa kusema kuwa hataogopa kamwe wale wanaopinga juhudi zake za maendeleo kwa kusema kuwa maendeleo ndiyo yalikuwa wazo lake kuu alipoamua kuwania kiti hicho.
“Tumeahidiana yakuwa tutaripoti yeyote ambaye anauza pombe haramu kwa polisi na pia tutaendeleza elimu maana hiyo ndiyo nguzo za maendeleo. Wakazi na vijana kwa ujumla wataanza kupata ajira kwa ushirikiano mwema na kampuni zilizokita kambi katika kaunti hii,” alisema Matuga.