Mwakilishi wa wadi ya Sensi katika eneo bunge la Kitutu Chache kaskazini Onchong’a Nyagaka ameombwa kukarabati daraja mbili za eneo la Riomuga Nyaora na ile ya Siera Nyantaro ili kurahisishia usafiri wa wakazi wa eneo hilo.
Wito huo umetolewa baada ya daraja hizo mbili kuwa katika hali mbaya kufuatia mvua nyingi iliyonyesha, huku wakazi wakipata muda mgumu kuvuka hadi ng’ambo ya pili na kulazimika kutumia njia tofauti ili kuvuka sehemu nyingine.
Wakizungumza na mwandishi huyu mnamo siku ya Jumanne katika eneo la Botobori, wakazi wa maeneo hayo waliomba msaada kutoka kwa mwakilishi wao ili kukarabati daraja hizo.
“Hatuna mahali pa kupita, kila siku tunalazika kupita mbali na ata watoto wanapoenda shule huwa vigumu na kuchelewa kufika shuleni kwa kupitia njia iliyo refu,” alisema mkazi mmoja.
“Tunaomba mwakilishi wetu kukarabati daraja hizo ili tuwe tunatumia kuvuka ng’ambo ingine na itakuwa kazi rahisi kwetu,” alisemea mkazi mwingine.
Wakati huo huo, wakazi hao waliomba mwakilishi kukarabati mito ya eneo la Nyabinyinyi Kiong’anyo na eneo la Nyansongo Sikonge ili kuwapa afueni ya maji safi.
Juhudi za kumtafuta mwakilishi huyo zilifua dafu na kuahidi kufanya hayo ila aliomba subira anapoendelea kupanga shughuli hizo