Mwakilishi wa Wadi ya Kongowea Jabez Mdhai ametiwa mbaroni kuhusuiana na utata katika umiliki wa magari mawili ya kifahari, ambayo inadaiwa anayamiliki na yadaiwa sio yake.
Akithibitisha kukamatwa kwake siku ya Ijumaa, afisa mkuu wa polisi eneo la Kisauni Walter Abondo alisema kuna madai ya kuwa mtu mmoja mwenye asili ya kigeni ameibiwa magari hayo, jambo lililopelekea Mdhai kutiwa mbaroni.
Abondo aliongeza kwa sasa wanachunguza kisa hicho kujua iwapo ni kweli magari hayo yamechukuliwa na mwakilishi huyo kwa kughushi stakabadhi za ununuzi.
Akizungumza na wanahabari katika makazi yake huko King'orani kabla ya kuchukuliwa na maafisa wa polisi wa kitengo cha mbwa, Mdhai alisema anayazuilia magari hayo kwa sababu mke wa mwenye magari hayo alishindwa kumlipa fedha alizomkopesha.
Kiongozi huyo amepinga madai ya kughushi stakabadhi za kumiliki magari hayo aina ya Harrier na Mercedes Benz.