Baadhi ya shule kutoka eneo la uwakilishi wadi ya Gesima huenda zikanufaika pakubwa kutokana na mpango wa mwakilishi wadi wa eneo hilo Atuti Nyameino kuanzisha mikakati ya kupeana mifuko ya simiti kwa shule mbalimbali katika eneo hilo.
Akihutubu kwenye hafla ya kuchangisha pesa kwenye eneo lake la uwakilishi siku ya Jumatatu, Atuti alisema kuwa shule nyingi katika eneo hilo zimekuwa zikiathirika pakubwa na funza, hali ambayo imemlazimu kuingilia kati kuhakikisha kuwa hali hiyo imerekebishwa.
Aidha, aliwahimiza wahisani kujitokeza kushirikiana naye ili kuhakikisha kuwa sakafu za shule husika zimekarabatiwa.
"Nitakuwa nikipeana mifuko kadhaa ya simiti kwa shule mbalimbali za umma ili zisaidie kukarabati sakafu zilizoko katika hali mbaya, na ni himizo langu kwa wahisani wajitokeze na kushirikiana nami ili kuhakikisha kuwa sakafu za shule mbalimbali zimekarabatiwa," alisema Nyameino.
Nyameino aidha aliipa changamoto wizara ya elimu kuweka mikakati kuhakikisha kuwa hali hiyo ya sakafu kuchipuka imerekebishwa, akiongezea kuwa afisi yake itasaidia shule kulingana na hali ya uharibifu wa sakafu akihoji kamati aliyoiteua kutoka kwa afisi yake imeanza kutembelea shule za umma ili kudadisi hali.
"Wakati sakafu za shule za umma zinapochipuka viongozi wakisiasa kutoka maeneo ya mashinani ndio wanao shtumiwa zaidi. Serikali ya kitaifa kupitia kwa wizara ya elimu inastahili kuweka mikakati yakukarabati sakafu hizo na tayari kamati yangu imeanza kutembelea shule mbalimbali ili tuone jinsi yakuzisaidia shule hizo," aliongezea Nyameino.