Wakulima kutoka wadi ya Nyansiongo kwenye kaunti ndogo ya Borabu wameombwa kupanda mimea na miti inayoweza kufanya vizuri hasa kwenye msimu huu wa mvua kubwa inayoendelea.
Akihutubu kwenye uwanja wa Nyansiongo mapema Jumatatu, mwakilishi wa wadi hiyo ambaye pia ni kiongozi wa wachache kwenye bunge la kaunti ya Nyamira Jackson Mogusu, alisema kuwa mvua ya El-nino inatarajiwa kunyesha katika eneo hilo hadi mwishoni mwa mwezi wa Decemba, huku akiwahimiza wenyeji kuchangamkia hali hiyo kwa kupanda miti na mboga, hatua itawafaidi siku za mbeleni.
"Mvua ya Elnino inatarajiwa kuisha mwishoni mwa mwezi Decemba, na nawasihi wakazi wa eneo hili kukumbatia kunyesha kwa mvua hii kubwa, na kupanda mboga pamoja na miti ili baadaye ije kuwafaidi pakubwa," alisema Mogusu.
Haya yanajiri baada ya shirika la utabiri wa hali ya hewa kutabiri kuwa kutakuwa na mvua kubwa, na kuwaweka tayari wananchi kutafuta mbinu za kukabiliana na changamoto zitakazosababishwa na mvua hiyo ambayo imekuwa ikinyesha katika sehemu mbalimbali nchini.