Share news tips with us here at Hivisasa

Mwaniaji kiti cha wadi ya Solai katika kaunti ya Nakuru Kelvin Waweru maarufu 'Kel Wesh' ametoa changamoto kwa vijana na akina mama wa eneo hilo ambao hawajajiandikisha kama wapiga kura kuhakikisha kwamba wanajiandikisha katika shughuli ya sasa inayoongozwa na tume huru ya uchaguzi na mipaka humu nchini IEBC.

Akizungumza katika hafla ya mazishi eneo hilo, Waweru alisema kuwa wakati ni sasa kwa vijana na akina mama kuhakikisha kwamba wanashiriki uchaguzi mkuu ujao na hili litawezekana tu iwapo watakuwa wamesajiliwa kama wapiga kura.

''Ningependa kuwarai vijana wa eneo hili la solai na hata akina mama kuhakikisha kwamba wanajisjili kama wapiga kura kwa ajili ya kuleta mabadiliko katika uchaguzi mkuu ujao," Waweru alisema.

Waweru ambaye alitangaza azma ya kuwania kiti hicho cha wadi ya Solai mapema mwaka huu alisisitiza kuwa wakati ni sasa wa vijana kuchukuwa hatamu za uongozi wa taifa hili.

Kwa mujibu wake swala la vijana kukosa ajira katika eneo hilo na taifa kwa jumla litatatuliwa tu iwapo vijana wenyewe watachagua viongozi ambao ni vijana na wanajali maslahi ya vijana.