Mwanaharakati wa kijamii na maswala ya uongozi Jackline Jebet amewasuta baadhi ya wanasiasa anaodai wanawahamisha wapiga kura kutoka sehemu moja hadi nyingine.
Katika mahojiano ya kipekee, Jebet alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kwa wanasiasa wanaojitakia umaarufu kuanza kuwasafirisha wapiga kura kutoka wadi moja hadi nyingine.
Mwanaharakati huyo kutoka wadi ya London Nakuru, amesema kuwa tayari amewasilisha swala hilo kwa afisi ya tume huru ya uchaguzi na mipaka humu nchini IEBC ili hatua mwafaka zichukuliwe.
"Ni jambo la kusikitisha kwamba viongozi wanawahamisha wapiga kura kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa kile kinaonekana ni kutafuta ushindi katika uchaguzi mkuu ujao," alidai Jebet.
Aliongeza kuwa huenda swala hilo likawagawanya wananchi kwa misingi ya kisiasa swala ambalo kwa mujibu wake ni pigo hasa ikizingatiwa kwamba kaunti ya Nakuru ina makabila yote.
Alitoa wito kwa viongozi kuhakikisha kwamba kuna amani na kukoma kuwagawanya wakenya kwa misingi ya kisiasa.