Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Huku mapigano baina ya jamii mbili katika mpaka wa Narok na Nakuru yakiendelea kushuhudiwa, mmoja wa wapiganiaji wa haki za binadamu amewataka rais Uhuru Kenyatta pamoja na Naibu wake kuchukua hatua za haraka na kuzuru eneo ambalo limeathirika.

Laurence Mwilu, ambaye ni mtetezi wa haki za watu waliotengwa kwenye jamii, kwenye mahojiano siku ya Jumatatu kwenye uga wa mapumziko wa Mama Ngina alisema kuwa serikali sharti ichukue wajibu na hatua ya mapema kabla ghasia hizo kusambaa kwenye Kaunti husika.

Mwilu aliwataka viongozi hao wawili kuwaongoza viongozi wengine wa kutoka Kaunti hizo husika na kuwakalisha viongozi wa koo za jamii hizo mbili na kuwaambia umuhimu wa kukaa pamoja kama ndugu na dada bila kuzingatia mahali mtu alizaliwa au asili yake.

Aidha, alisema kuwa huenda kuna baadhi ya viongozi wa kisiasa ambao wana mkono kwenye ghasia hizo za kikabila, na kusihi mamlaka ya maridhiano na utangamano nchini kwa ushirikiano wa idara za usalama kuchunguza iwapo kuna mtu yeyote ambaye amehusika katika kuchochea ghasia.

“Idara ya polisi na tume ya maridhiano na utangamano nchini sharti iwe macho na iliangazie swala hili mapema, na wale ambao wanahusika kunaswa na kushtakiwa dhidi ya makosa hayo,” aliongeza Mwilu.