Mahakama imempa mwanamke anayedaiwa kupanga njama ya kumuua mumewe dhamana ya Sh500,000.
Rose Adhiambo ambaye ni mke wa Polycarp Okumu, akiwa ameshirikiana na mfanyikazi wake wa nyumbani Doris Akinyi wanadaiwa kupanga njama na majambazi kumvamia Okumu katika eneo la Nyali kati ya Oktoba 20 na Oktoba 26, 2015.
Akitoa dhamana hiyo siku ya Alhamisi, Hakimu Henry Rotich alisema kuwa dhamana hiyo itakuwa funzo kwa wengine wanaojihusisha na visa kama hivyo.
Hii ni baada ya wakili Gikandi Ndibuini kuiomba mahakama kuwaachilia wateja wake kwa dhamana kwani ni haki yao kikatiba.
Siku ya Jumatano meneja wa kampuni ya ulinzi ya kibinafsi ya Guard Force Group Debra Otigo alitozwa dhamana ya Sh500,000 kwa tuhuma za mauaaji ya mfanyibiashara huyo Polycarp Okumu.
Kufikia sasa washukiwa wanne wametiwa mbaroni na kufunguliwa mashtaka kwa kuhusishwa na njama hiyo ya mauaaji.