Mwanamke mmoja anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kondele jijini Kisumu, kwa tuhuma za kumuua mume wake.
Taarifa zaidi zimearifu kuwa mwanamke huyo anadaiwa kumuua mumewe Samwel Maraga nyumbani kwao katika eneo la White House mtaani Manyatta jijini Kisumu, kwa kumdunga kisu mara kadhaa tumboni baada ya kuibuka mvutano wa kifamilia kati yao.
Kisa hiki kimethibitishwa na chifu wa eneo husika Miduri Ojowi.
OCS wa kituo cha polisi cha Kondele Baraza Khan, amesema mwili wa mwendazake uliopatikana chumbani mwake, utafanyiwa upasuaji ili kubaini chanzo kamili cha kifo chake.
''Kwa sasa mshukiwa amezuiliwa huku tukisubiri ripoti ya upasuaji itakayoelezea bayana sababu ya kifo cha mwendazake,'' aisema Khan.
Mwili wa mwenda zake, unahifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga almaarufu Russia jijini Kisumu, huku ukisubiri kufanyiwa upasuaji.