Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wito umetolewa kwa wanandoa katika wilaya pana ya Molo kutumia njia za kisheria kusuluhisha tofauti za ndoa, badala ya kuvamiana.

Hii ni baada ya mwanamme mwenye umri wa makamo kulazwa katika hospitali ya wilaya ya Molo Jumatano akiwa na majeraha mabaya baada ya kukatwa kwa upanga na mkewe kufuatia mzozo wa kinyumbani.

Mzee huyo, baba wa watoto watatu kutoka kijiji cha Kiambiriria, alikatwa kwenye kichwa na mguu, pale ugomvi ulipozuka kuhusu matumizi ya pesa walizokuwa wameuza viazi. 

Mama huyo alidai mumewe ametumia fedha hizo kwa ulevi na starehe na wanawake.

Bwana huyo alisema baada ya kupatilizwa kichapo kikali, mkewe alichukua upanga kwa hasira na kumkata kwenye kichwa pamoja na mguu wake wa kulia.

“Pesa zenye nilikuwa nimefanyia kazi ndizo nilikunywa, na tulikuwa tumeuza viazi vya elfu mbili, lakini nilikuwa mlevi nikapata amenikata,” alisema bwana huyo.

John Towett, mkaazi wa eneo hilo ambaye pia ni jirani alisema waliskia mayowe kutoka kwa jamaa huyo, na wakamkimbiza hospitalini baada ya kugundua kilichotendeka. 

Towett alitoa wito kwa wazee kutopelekea ‘ndogo ndogo pesa’ haswa msimu huu wa krisimasi, na pia kuwashauri akina mama kutunza wazee.

Polisi wanaendelea kuchunguza kisa hicho huku madaktari kwenye hospitali ya Molo wakisema afya ya mwadhiriwa inaimarika.