Mwanamume mmoja alipoteza maisha yake usiku wa kuamkia siku ya Alhamisi baada ya kukanyagwa na lori katika eneo la Kakuku, Ithanga, katika Kaunti ya Machakos.
Akidhibitisha kisa hicho, chifu wa Ithanga Bwana Josphat Kilee alisema kuwa lori hilo lilishindwa kupanda mlima, pale ambapo mwanamume huyo alishuka kutoka lori hilo kuliwekea jiwe ili kulizuia kurudi nyuma linapopanda mlima huo.
Kilee alisema kuwa lori hilo lilirudi nyuma na kumkanyaga mwanamume huyo kichwani na mabegani, na akaaga dunia papo hapo.
Chifu huyo aliwataka madereva wa lori kuwa makini wafikapo kwenye milima ili kuzuia majanga kama hayo.
Mwili wa mwanamume huyo ulipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Thika level five.