Mwanamume anayedaiwa kujihusisha na utoaji wa matibabu kwa mifugo bila ya idhini ya bodi husika alifikishwa kwenye mahakama ya Nakuru siku ya Jumatatu kujibu shtaka hilo.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa mshtakiwa, Joseph Odhiambo, alikuwa akiendeleza biashara hiyo katika duka moja la kuuzia dawa la Bahati Farm Care Agrovet, lilioko Maili Kumi, viungani mwa mji wa Nakuru tarehe Mei 18, 2015.
Akitoa ushahidi mahakamani, Dkt Idraph Ragwa, wa bodi ya kitaifa ya utabibu wa mifugo (Kenya Veterinary Board) alieleza mahakama kuwa alikuwa ameandamana siku hiyo na maafisa wawili wa polisi wa utawala wakiendesha ukaguzi wa maduka ya kuuza dawa za mifugo katika Kaunti ndogo ya Bahati.
Dkt Ragwa alielezea kuwa walifika katika duka hilo na kupata mshtakiwa akiendesha biashara hiyo kinyume cha sheria kwani hakuwa na leseni ya kumwidhinisha kufanya biashara hiyo, kutoka kwa bodi ya utabibu wa mifugo.
Kulingana naye, hilo liliwapelekea kumkamata mshukiwa na kumfikisha katika Kituo cha polisi cha Bahati.
Mshtakiwa huyo kupitia kwa wakili wake alimtaka daktari huyo kutoa ushahidi wa kudhibitisha madai yake mbele ya korti.
Upande wa mashtaka nao umeomba mahakama muda ili kuwasilisha mashahidi wengine wawili mahakamani, ambao wanahusika katika uendeshaji wa mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne wa KCSE.
Kesi hiyo iliyowasilishwa mbele ya Hakimu Mkuu Liz Gicheha na itaendelea tarehe Februari 2, 2016.