Share news tips with us here at Hivisasa

Mwanamume wa umri wa makamo amefungwa kifungo cha miaka 20 gerezani kwa kumuua mkewe.

Mdoe Dewa Kombe anadaiwa kutekeleza mauwaji hayo kwa kumkatakata mkewe, Kwekwe Nyanje, mnamo Oktoba 14, 2011 katika mtaa wa Majengwani lokesheni ya Wereni, Kaunti ya Kwale.

Kombe aliambia mahakama kwenye usahidi wake kuwa alipandwa na hasira baada ya kumpata mkewe akishiriki ngono na mwanamume mwengine ndani ya nyumba yake, ndiposa akajipata amemkatakata kwa panga hadi akaaga dunia.

Akitoa hukumu hiyo siku ya Jumatatu, Jaji Martin Muya alisema kuwa ushahidi uliotolewa ulionyesha kuwa Kombe alihusika pakubwa katika mauwaji ya mkewe.

Muya aliongeza kuwa hukumu hiyo itakuwa funzo kwa wengine wanaojihusisha na visa vya mauwaji nchini.

“Hukumu hii itakuwa funzo na onyo kwa wale wanaojihusisha na mauwaji kiholela holela nchini,” alisema Jaji Muya.

Kombe alipewa siku 14 za kukata rufaa kupinga kifungo hicho.